Kuitwa kuteseka na kufurahi: Kukamilisha lengo la mateso ya Kristo
Kutoka Gospel Translations Swahili
By John Piper
About Suffering
Part of the series Called to Suffer and Rejoice
Translation by Desiring God
Sasa nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu na katika mwili wangu ninatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, ambao ni kanisa. 25 Mimi nimekuwa mtumishi wa kanisa kwa wajibu aliyonipa Mungu ili kuwaletea ninyi neno la Mungu kwa ukamilifu. 26 Siri hii ilikuwa imefichika kwa karne nyingi na vizazi voingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu. 27 Kwao, Mungu amechagua kujulisha miongoni mwa watu wa mataifa utukufu wa utajiri wa siri hii, ambayo ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu. 28 Yeye Kristo ndiye tunayemtangaza, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu kwa hekima yote ili tuweze kumleta kila mmoja akiwa amekamilika katika Kristo. 29 Kwa ajili ya jambo hili, ninajitaabisha, nikijitahidi kwa kadiri ya nguvu zile ambazo kwa uwezo mwingi hutenda kazi ndani yangu.
Nataka tuangazie mstari wa 24 na Paulo “akitimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo.” Yawezekanaje kitu kinaweza kuwa kimepungua katika mateso ya Kristo? Je mateso na kifo chake kwa ajili yetu hakikutosha kwa yote? Basi anamaanisha nini katika mstari 24 na inatuhusu kwa njia gani?
Yaliyomo |
Kufupisha aya hii
Lakini ilikuona mstari wa 24 kwa njia mwafaka wacha tukauangalie uhusiano wake na mistari inayosalia. Tukianza na mstari wa 29 wacha turudi nyuma na kujumulisha yale Paulo anayoyasema katika aya hii.
Mstari wa 29; Paulo ansema kuwa kuna sababu ya kumfanya ajitaabishe. Na ni jitihada, na kutaabika, katika kazi hii si kwa nguvu zake tu. Ni uwezo mwingi ambao unatenda kazi ndani yake.
Mstari wa 28 unaeleza lengo la kujitahidi kwa Paulo, ambalo ni kuweza kumleta kila mmoja akiwa “amekamilika katika Kristo.” Na anatenda hili kwa kumtangaza Kristo, akimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu. Hii ni jitihada ya Paulo bila kukoma ambao amepewa kwa uweza wa Kristo.
Mistari 26-27 inaeleza kwa wazi zaidi yale Paulo anatangaza na kuyafundisha. Linaitwa ‘siri’ katika mstari wa 26, si kwamba haliwezi kueleweka, bali imefichika kwa karne nyingi na vizazi vingi, lakini sasa imefunuliwa kwa watakatifu. Halafu mstari wa 27 unaeleza utajiri wa utukufu wa siri hii. “Ni Kristo ndani yenu[watu wa mataifa], tumaini la utukufu.” Lile ambalo halikuwa limefunuliwa kabisa kwa karne nyingi na vizazi vingi lilikuwa Mwokozi wa Wayahudi—Krist—atawafikia hata mataifa yasiyo ya Wayahudi na kuishi kati ya wasio Wayahudi. Kwa hakika ataishi miongoni mwao na kuwapa ahadi ya Abrahamu, tumaini la utukufu katika Ufalme wa Mungu pamoja na watakatifu wote.
Lakini sasa siri inafunuliwa na Paulo anatangaza Kristo na kuhubiri kila pahali kuwa kuishi kwa Masiya na tumaini la utukufu wa Mungu ni kwa wote wanaotumaini Kristo na hakika wanatumaini katika utukufu wa Mungu (1:4, 23).
Mstari wa 25 unasema kuwa tangazo hili la Kristo ni utimilifu wa wajibu ambao Mungu amempatia Paulo kutangaza Neno Lake. Ni mtumishi wa kanisa na mhudumu wa Mungu. Jukumu lake ni kupeleka Neno la Mungu kwa mataifa, na kuwapa tumaini la utukufu, na kuwaita kwa imani. Na basi ni mhudumu wa kanisa kwa kusanya wateule wa Mungu kutoka kwa mataifa, na kuwafundisha na kuwaonya ili wapelekwe kwa ukamilifu kwa Kristo.
Mstari wa 24 unasema kuwa huduma hii ya kuendeleza siri ya Kristo na tumaini la utukufu kwa mataifa, na halafu kuonya, na kuwafundisha ina mateso. “Sasa nafurahi kuteseka kwangu kwa ajili yenu na katika mwili wangu ninayatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake (ambao ni kanisa).
“Kutimiliza yale yaliyopungua” yamaanisha nini?
Sasa hii inamaanisha nini Paulo anapoteseka kwa ajili ya kanisa—kuendeleza tumaini la utukufu kwa watu wengine wengi, na kuwafundisha juu ya siri ya Kristo, na kuteseka anapofanya hivi— “Anatimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo”? je mtu yeyote anawezaje kutimiliza yale yaliyotosha vile kuteseka kwote kunaweza kuwa?
Muktadha unadokeza maana
Nadhani andiko ambalo tumeliangalia tu sasa hivi lamaanisha kuwa mateso ya Paulo yatimiliza Kristo si kwa kuongeza chochote katika thamani yao, lakini kwa kuyaendeleza kwa watu ambao yalitakikana yabariki. Yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo si kwamba yamepungukiwa kwa thamani ama kiwango, ni kana kwamba hayangetosha kufunika dhambi ya wote wanaoamini. Yale yaliyopungua ni ile thamani isiyokoma ya mateso ya Kristo ambayo hayajajulikana kwa walimwengu. Bado ni siri (yamefichika) kwa watu wengi. Na lengo la Mungu ni kuwa siri ipate kufunuliwa na kuendelezwa kwa watu wa Mataifa. Basi mateso yamepungua kwa njia ya kwamba hayaonekani wala kujulikana kwa mataifa. Lazima yabebwe kwa huduma ya neno. Na wahudumu wa neno wanatimiliza yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa kuyaendeleza kwa wengine.
Maneno sawia katika Wafilipi 2:30
Kuna dhibitisho ya nguvu yah ii kwa matumizi ya maneno sawa katika Wafilipi 2:30—. Kuna mtu ambaye jina lake lilikuwa Epafrodito katika kanisa la Filipi. Wakati kanisa la huko walipokusanya msaada kwa Paulo (labda pesa, ama vitu vya kupeana ama vitabu), waliamua kuutumia Paulo huko Roma kwa mikono ya Epafrodito. Katika safari yake akibeba vitu hivi karibu anapoteza maisha yake. Mstari wa 27 unasema, alikuwa mgonjwa karibu ya kufa, lakini Mungu alimhurumia.
Halafu katika mstari wa 29 Paulo anawaambia kanisa ya Filipi kumpokea Epafrodito katika Bwana kwa furaha kubwa, na anapeana sababu yake katika mstari wa 30 ulio na maneno sawa na Wakolosai 1:24. “Kwa sababu alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, akihatarisha maisha yake kukamilisha [kusema kutimiliza] yaliyokosekana [yaliyopungua] katika kazi yenu kwangu. Sasa katika neno kamili “kukamilisha yaliyokosekana” katika kazi yenu kwangu ni karibu sawa na “ kutimiliza yaliyopungua” katika mateso ya Kristo katika Wakolosai 1:24.
Ni kwa hali gani, basi, huduma ya wafilipi kwa Paulo “ilkuwa na upungufu” na kwa hali gani Epafrodito “aliyatimiliza” yaliyokuwa yamepungua kayika huduma yao? Miaka mia moja iliyopita mtu wa kutoa maoni, Marvin Vincent, nadhani unaipata kwa njia mwafaka.
Zawadi ya Paulo ilkuwa zawadi kwa kanisa kama mwili. Ilkuwa toleo la dhabihu ya upendo. Kile kilikuwa kimepungua, na kile kingekuwa shukrani kwa Paulo na kanisa pia, kilikuwa kuwasilishwa kwa toleo hili kwa kupitia mikono ya mtu. Hii ilkuwa haiwezekani, namna Paulo anawakilisha Epafropdito kama anayetimiliza upungufu huu kupitia upendo wake na huduma yenye shauku. (Barua kwa Wafilipi na Filemoni, ICC ukurasa 78)
Vile tunatimiliza yaliyopungua katika mateso ya Kristo
Nadhani hivyo ndiyo maneno yanavyomaanisha katika Wakolosai 1:24 pia. Kristo ameandaa toleo la upendo kwa ulimwengu kwa kuteseka na kufa kwa ajili ya wenye dhambi. Ni kamili na haijapungukiwa na chochote—ilhali tu kitu kimoja, kuwasilishwa moja kwa moja na Kristo mwenyewe kwa mataifa ya dunia na watu mnaofanya nao kazi pahali pamoja. Jibu la Mungu kwa upungufu huu ni kuita watu wa Kristo (watu kama Paulo) kuwasilisha mateso ya Kristo kwa ulimwwengu—kuyabeba kutoka Yerusalemu hadi mwisho wa dunia.
Kwa hii tunatimiliza yaliyopungua katika mateso ya Kristo. Tunakamilisha yale yaliyokusudiwa kwayo, kusema, kuyawasilisha moja kwa moja kwa watu wa ulimwengu ambao hawajui kuhusu thamani isiyokoma.
Lakini tazama vile Paulo anavyosema katika mstari wa 24. Anasema kwamba ni katika mateso yake na mwili wake—ni kusema, mwili wake mwenyewe unaoteseka ambao unafanya upande wake wa kutimiliza mateso ya Kristo. Basi Paulo anaona uhusiano wa karibu kati ya mateso yake na ya Kristo. Kile hiki kinamaanisha, nadhani, ni kuwa Mungu anakusudia mateso ya Kristo yawakilishwe kwa ulimwengu kupitia mateso ya watu wake. Mungu anamaanisha kwa mwili wa Kristo, ambaye ni kanisa, kushuhudia baadhi ya mateso aliyoyapata ndipo tunapopeana Kristo wa msalaba kwa watu, wanamwona ndani yetu. Yatupasa tufanye mateso ya Kristo kuwa hakika kwa watu kupitia mateso tunayoyapata kwa kuwapatia Yeye, na kuishi maisha ya upendo aliyoishi.
“Nafurahia kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu . . . kutimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo.” Kristo anapenda kuwa na uwakilishi wa moja kwa moja ya mateso yake kwa ulimwengui. Na njia anayomaanisha kujitolea kama anayeteseka kwa ajili ya ulimwengu na kwa ulimwengu ni kupitia watu wake ambao, kama Yeye, wako tayari kuteseka kwa ajili ya ulimwengu. Mateso yake yamekamilika katika kuteseka kwetu kwa sababu kupitia kwa mateso yetu walimwengu wanaona mateso yake, na wanazo athari zao zilizoteuliwa. Upendo wa mateso ya Kristo kwa ajili ya wenye dhambi unaonekana katika upendo wa mateso ya watu wake kwa ajili ya watenda dhambi.
Nadhani yale tunayaona katika Wakolosai 1:24 ni kuishi kupitia Neno lake Yesu katika Marko 8:35, “kwa maana mtu yeyote anyetaka kuokoa nafsi atipoteza, lakini yule apotezaye maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili ataiokoa.” Njia ya wokovu ni njia ya kupoteza maisha ya mmoja kwa ajili ya injili. Hoja ni kwamba kupeleka injili kwa watu (kwa ofisi ama ng’ambo ya bahari) kwa kawaida yahitaji kujinyima na kuteseka, kupoteza kwa maisha ama kujikana mwenyewe. Hii ndio njia Kristo amemaanisha kwa ajili ya mateso yake iokoayo kupelekwa kwa ulimwengu, kupitia mateso ya watu wake.
Furaha ya Paulo katika mwito huu
Na Paulo anasema anafurahi kwa haya. Mstari wa 24 “Sasa nafurahi kule kuteseka kwangu kwa ajili yenu.” Njia ya Kalvari si njia isiyokuwa na furaha. Ni njia ya machungu, lakini iliyo na furaha tele. Tunapochagua msururu wa utamu wa starehe na ulinzi juu ya kujinyima na mateso ya huduma na mahubiri na upendo, tunachagua kinyume na furaha. Tunachagua mabirika yanayovuja ambayo hayawezi kuifadhi maji na kuyakataa chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe (Isaya 58:11).
Watu wenye furaha zaidi ulimwenguni ni wale wanaojua siri ya Kristo ndani mwao, tumaini la utukufu unaotoshelesha tamaa yao ya ndani na kuwaweka huru ili waendeleze mateso ya Kristo kupitia kwao wenyeyewe kwa ulimwengu.
Mungu anatuita katika andiko hili kuishi kwa ajili ya Injili na kufa kupitia mateso. Kristo alichagua mateso, hayakufanyika tu kwake. Aliuchagua kama njia ya kuumba na kufanya kamilifu kanisa. Sasa anatuita tuchague mateso. Ni kusema, anatuita tujitwike msalaba wetu na kumfuata katika njia ya Kalvari na kujikana na kujitolea kwa ajili ya kuwakilisha mateso yake kwa ulimwengu na kulihudumia kanisa.
Nilisikia njia ya kumbu kumbu ya kusema haya kutoka kwa mchungaji wa Kirumi na mkuu wa huduma Joseph Tson. Alisema, “ Msalaba wa Kristo ilkuwa ya neema; yetu ni ya ongezeko.” Ni kusema, Kristo aliteseka kutimiliza wokovu; tunateseka kueneza wokovu. Na kuwa kwetu tayari kuvumilia majanga kwa wema wa wengine ni kutimiliza mateso ya Kristo kwa sababu inayaendeleza kwa wengine na kuyafanya yaonekane.
Hadithi ya mhudumu mwenye asili ya kihindi
Nilipokuwa nikitayarisha kitabu cha huduma mwezi wa Mei nilipata fursa ya kusikia J. Oswald Sanders akiongea. Ujumbe wake uliniguza kwa undani juu ya mateso. Ana umri wa miaka 89 na bado anasafiri na kuhubiri katika ulimwengu. Ameandika kitabu tangu afikishe umri wa miaka 70! Nataja hiyo ili tu kuinua bidii yote ya maisha iliyomwagwa kwa ajiili ya injili bila kujali kuwa katika hali ya kujitunza kwanzia umri wa miaka 65 hadi kaburini.
Alikariri hadithi ya mhudumu wa kijijini ambaye alitembea mguu mtupu kutoka kwa kijiji kimoja hadi kingine akihubiri Injili kule nchini India. Matatizo yake yalikuwa mengi. Baada ya siku mrefu ya hatua nyingi na kukata tamaa kwingi aliwasili katika mji fulani na kujaribu kuhubiri Injili lakini alifukuzwa nje ya mji na kukataliwa. Basi akaenda kando ya mji akiwa ameudhika na kujilaza chini ya mti na kulala kutokana na uchovu.
Wakati aliamka, watu walikuwa wamemzingira, na mji mzima ulikuwa umekusanyika kusikia yale aliyotaka kuyasema. Mkuu wa kijiji akamweleza kuwa walikuja kumchunga alipokuwa amelala. Walipoona miguu yake ilivyokuwa imechubuka, walijua kuwa lazima awe ni mtu mtakatifu, na walikuwa waovu kumkataa. Walimwomba radhi na walitaka kuusikia ujumbe ambao alikuwa tayari kuteseka kwayo ili awaletee.
Basi mhubiri alitimiliza mateso ya Yesu kupitia miguu yake mizuri iliyochibuka.
Hadithi ya shujaa wa Kimasai aitwaye Yosefu
Mojawapo wa watu wa kutotarajiwa kuhudhuria Kongamano la wahubiri walio na Mpangilio huko Amsterdam iliyodhaminiwa na Kikundi cha Billy Graham alikuwa mpiganaji wa Kimasai aitwaye Yusufu. Lakini hadithi yake ilimfanya asikizwe na Daktari Billy Graham mwenyewe. Hadithi inakaririwa na Michael Card. 1
Siku moja Yosefu, ambaye alikuwa akitembea katika mojawapo ya barabara ya Kiafrika iliyo na vumbi na joto, alikutana na mtu fulani aliyeshiriki pamoja naye Injili ya Yesu Kristo. Papo hapo alikubali Yesu kama Bwana na Mwokozi wake. Nguvu za Roho zikaanza kugeuza maisha yake; alijawa na furaha ambapo kitu cha kwanza alichotaka kufanya illikuwa kurudi kijini mwake na kushiriki na watu wa ukoo wake hiyo habari njema.
Yosefu alianza kuenda kwa mlango moja hadi nyingine, akimwambia kila mtu kuwa alikutana na msalaba [mateso] wa Yesu na wokovu iliyokuwa ikipeana, akitarajia kuona nyuso zao zikiingia vile yake ilikuwa. Kwa mshangao wake watu wa kijiji hawakujali tu, bali waligeuka wakali. Wanaume walimshika na kumweka chini kwa mchanga huku wanawake wakimchapa na nyaya za seng’enge. Alivutwa nje ya kijjiji na kuachwa afe pekee yake katika msitu.
Yosefu aliweza kutambaa hadi katika kisima cha maji, baada ya kuzirai kwa siku kadhaa na kupooteza fahamu, akapata nguvu ya kuinuka. Alishtushwa na makaribisho makali aliyoyapata kutoka kwa watu aliyokuwa amewajua maishani mwake mwote. Baada ya kufanya mazoezi ya ujumbe ambao alikuwa ameusikia hapo mwanzo, aliamua kurudi na kushiriki imani yake kwa mara nyingine.
Yosefu akalegea katika msururu wa nyumba kutangaza Yesu. “Alikufa kwa ajili yako, ndipo upate kupokea msamaha na upate kujua Mungu aishiye” aliwasihi. Tena alikamatwa na wanaume wa kijiji, na kufungwa huku wanawake wakimpiga na kuviumiza tena vidonda vyake ambavyo vilikuwa vimeanza kupona. Kwa mara nyingine akiwa amepoteza fahamu nje ya kijiji na kumwacha afe.
Kuponea kifo cha kwanza kulikuwa ya ajabu. Kuponea kwa mara ya pili kulikuwa muujiza. Tena, baada ya siku kadhaa baadaye, Yosefu aliamka misituni, akiwa ameburushwa, na akiwa na makovu—na akiwa na shauku ya kurudi. Alirudi kwa hicho kijiji kidogo na wakati huu, walimvamia kabla ya kupata fursa ya kufungu kinywa chake. Walipokuwa wakimpiga kwa mara ya tatu na yawezekana mara ya mwisho, tena akawaongelesha juu ya Yesu Kristo, Bwana. Kabla ya kuzirai, kitu cha mwisho alichoona ni wanawake waliokuwa wakimpiga wakiangua kilio.
Wakati huu aliamka kwa kitanda chake. Wale waliompiga sana sasa ndio wale wale waliokuwa wakijaribu kuokoa maisha yake na kumtunza ili arudi katika hali nzuri ya kiafya. Kijiji chote walimjua Kristo. Hii ni mfano moja wazi ya yale Paulo aliyamaanisha aliposema natimiliza yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake.
Kuna kitu fulani kinachoweka huru kabisa na kudumisha kwa kujua kwamba Kristo anatuita ili tujikane kwa ajili ya injili. Inatudumisha kutoka kwa kushtuliwa wakati inapokuja. Na inatufanya tuwe huru kuchagua wakati inatujia. Na inaanza kutuweka huruu kutoka kwa utongozaji wa ustawi wa Kimarekani.
Hadithi ya upeanaji wa kidhabihu huko nchini Haiti
Ni karibu vigumu sana kwa Wamarekani kukubaliana na sifa za Yesu kwa mjane ambaye “katika ufukara wake wote alipeana vyote alivyokuwa navyo.” (Luka 21:4). Hakika alimsifu. Hakumshtaki kwa kutoajibika kwake. Alisifu kujitolea kwake kwa ajili ya Mungu. Ili kuona Roho hii ikidhihirishwa nje, tunaweza kutoka Marekani na kuenda kwingine. Stanford Kelly anaikariri kutoka Haiti.2
Kanisa lilikuwa na sherehe ya kurudisha shukrani na kila Mkristo alialikwa kuleta toleo la upendo. Bahasha moja kutoka kwa mtu mwenye asilia ya Kihiti aitwaye Edmund ilikuwa na dola 13 pesa taslimu. Hiyo ilikuwa pesa inayotoshana na mshahara ya mtu ambaye amefanya kazi kwa miezi mitatu huko. Kelly alishangazwwa kama vile wale wanaohesabu sadaka ya Jumapili huko Marekani wanaweza, kupata zawadi ya dola 6000 pesa taslimu. Alitafuta Edmund, lakini hakuweza kumwona.
Baadaye Kelly alikutana naye kule kijijini na akamuuliza. Alimsukuma akamwelezee sababu na kupata kuwa Edmund alikuwa ameuza farasi yake ili apate kupeana zawadi ya dola 13 kwa Mungu kwa ajili ya injil. Lakini kwa nini hakuja kwa sherehe? Alisita na hakutaka kujibu.
Hatimaye Edmund akasema, “sikuwa na nguo ya kuvaa.”
Kile tunaona katika wiki hizi ni kuwa Mungu anatuita ili tujiandae kuteseka . . . si tu kwa sababu ya athari ya kimaadili ya utakaso na kufanywa wepesi; na si tu kwa sababu ya mambo ya kindani ya kuingia ndani na Yesu na kumjua vyema; lakini pia kwa sababu yale yaliyopungua katika mateso ya Kristo lazima yatimilizwe na wala wanaopeleka mateso hayo kwa ulimwengu na kuonyesha dhabihu ya upendo wa Kristo kupitia dhabihu ya upendo kwa watu wake.
1 Michael Card, "Wounded in the House of Friends," Virtue, March/April, 1991, pp. 28–29, 69.
2 Norm Lewis, Priority One: What God Wants (Orange, California: Promise Publishing, 1988), p. 120.